Waziri wa mambo ya nje wa Urusi Sergei Lavrov amekutana na kiongozi wa Korea Kaskazini Kim Jong Un, wizara ya mambo ya nje ya Urusi ilisema siku ya Alhamisi, huku nchi hizo mbili zikijenga uhusiano wa karibu zaidi katika kukabiliana na kile wanachokiona kuwa kambi ya Magharibi yenye uhasama na uchokozi inayoongozwa na Marekani.
Shirika la habari la serikali ya Urusi TASS liliripoti kuwa mkutano wa Lavrov na Kim ulidumu kwa zaidi ya saa moja lakini wizara haikutoa maelezo zaidi.
Lavrov, ambaye aliwasili Pyongyang siku ya Jumatano, awali aliishukuru Korea Kaskazini kwa kuunga mkono hatua za kijeshi za Urusi nchini Ukraine na kuahidi “msaada kamili wa Moscow na mshikamano” kwa Kim, wizara ya mambo ya nje ya Urusi ilisema.
Ziara ya Lavrov inaonekana kuandaa mazingira ya ziara ya Rais Vladimir Putin, ambaye ameongeza ushirikiano na Korea Kaskazini iliyotengwa kisiasa.
Akizungumza katika tafrija iliyoandaliwa na Kaskazini Jumatano, Lavrov alisema Moscow inathamini sana “uungaji mkono usioyumba na wa kanuni” wa Pyongyang kwa Urusi katika vita vya Ukraine, ambavyo inaviita “operesheni maalum ya kijeshi”.
“Kadhalika Shirikisho la Urusi linapanua msaada wake kamili na mshikamano na matarajio ya DPRK,” Lavrov alisema, kulingana na nakala ya hotuba iliyotolewa kwenye tovuti ya wizara yake.
DPRK ni herufi za kwanza za jina rasmi la Kaskazini, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Watu wa Korea.