Msemaji wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Stephane Dujarric amesema tangu mapigano yaibuke nchini Sudan Aprili 15, watu takriban elfu nne wameuawa na wengine maelfu wamejeruhiwa huku wafanyakazi wa kibinadamu wa Umoja wa Mataifa wakisema mapigano hayo pia yamesababisha maelfu ya watu kukimbilia nchi jirani za Sudan Kusini na Chad.
Dujarric ameongeza kuwa Shirika la Kuhudumia Wakimbizi la Umoja wa Mataifa UNHCR na washirika wake, wametoa vifaa vya msingi vya msaada kwa familia za wakimbizi kaskazini na magharibi mwa Darfur, na pia Umoja wa Mataifa unaendelea kutoa wito kwa pande mbalimbali za mgogoro huo kuhakikisha ulinzi wa raia na upatikanaji wa misaada ya kibinadamu katika maeneo inapohitajika.
Hadi sasa zaidi ya watu 700,000 wamekoseshwa makazi ndani ya nchi kutokana na mapigano ambayo yamekuwa yakiendelea kwa wiki ya nne, Paul Dillon, msemaji wa Shirika la Kimataifa la Uhamiaji, alisema mjini Geneva.
Hata kabla ya mapigano kuanza, watu milioni 3.7 waliandkishwa ni wasiokuwa na makazi ndani ya nchi.