Kiongozi wa jeshi la Gabon Brice Oligui Nguema ameachana na mshahara wake kama rais na atapokea tu mshahara kama kamanda wa walinzi wa jamhuri.
Alikua rais wa muda kufuatia kupinduliwa kwa Rais Ali Bongo mwezi Agosti mwaka huu.
msemaji wa junta katika tangazo Jumatano alisema Jenerali Nguema alichukua uamuzi huo kwa sababu “anafahamu dharura za kijamii na matarajio mengi ya watu wa Gabon”.
“Kila siku inayopita inaruhusu [junta] kufahamu zaidi hali ya jumla ya kuzorota kwa nchi na hasa fedha za umma,” Kanali Ulrich Manfoumbi alisema katika ripoti ya BBC.
Utawala wa miaka 14 wa Rais Bongo aliyeondolewa madarakani uligubikwa na madai ya ufisadi na kashfa nyingine za kifedha, huku serikali ikisema kuwa fedha za nchi hiyo ni “waathirika wa ghadhabu halisi ya uhalifu”.
Mbali na kukataa mshahara wake kama rais, Jenerali Nguema pia aliamua kupunguza matumizi ya fedha za umma kwa kupunguza posho za wabunge, kuondoa fedha za kisiasa na kukata posho za vikao.