Naibu waziri Mkuu na Waziri wa Nishati Mhe. Dkt. Doto Biteko amesema kuwa hali ya utoshelevu wa mafuta nchini kwa kipindi cha mwezi Julai hadi Septemba ni ya kuridhisha na Serikali kupitia Wakala wa Uagizaji wa Mafuta kwa Pamoja (PBPA) inaendelea kuingiza mafuta kwa mujibu wa taratibu na mikataba iliyowekwa na kukubalika.
Dkt.Biteko amesema hayo tarehe 19 Oktoba 2023 jijini Dodoma wakati Wizara ya Nishati ilipokuwa ikitoa taarifa kwa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti kuhusu hali ya uagizaji wa mafuta nchini pamoja na upatikanaji wa fedha za kigeni
“Ujazo wa mafuta yaliyokuwepo nchini kwa ajili ya matumizi ya ndani mwishoni mwa mwezi Septemba, 2023 yalikuwa ni jumla ya lita 248,815,232 ikiwa ni lita 136, 532,747 za dizeli, lita 93,305, 815 za petroli na lita 18,978, 670 za mafuta ya ndege na taa” amesema Mhe Dkt Biteko
Aidha, amesema kuwa, bakaa hiyo ya mafuta inajumuisha mafuta yaliyokuwepo katika maghala ya mafuta na yale yaliyokuwa katika hatua za upakuaji na wastani kila wakati kumekuwa na ziada ya mafuta isiyopungua siku 15 kwa dizeli na petroli wakati ambapo kwa Mafuta ya ndege ziada huzidi siku 30.
Kuhusu suala la upatikanaji wa Fedha za kigeni nchini, Waziri wa Fedha, Mhe. Dkt Mwigulu Nchemba amesema kuwa, sababu za uhaba wa Fedha za kigeni umechangiwa na athari za uviko-19, kwa kusababisha ukuaji wa uchumi wa mataifa mbalimbali duniani ambapo wa Tanzania ulikuwa kwa takriban asilimia 4.9 , mdororo wa kiuchuni uliosababishwa na kufungwa kwa baadhi ya shughuli za uchumi kama vile China, na Athari za Vita ya Ukraine na Urusi na hivyo kusababisha ongezeko la bei katika soko la dunia, mabadiliko ya tabia ya nchi na ongezeko la riba nchini Marekani na hivyo kusababisha mahitaji makubwa ya Fedha ya kigeni hususani Dola za Marekani.
Amesema, Tanzania imechukua hatua mbalimbali kukabiliana na upungufu huo ikiwa ni pamoja na kuziagiza Wizara kuunda timu ya wataalamu kufanya upembuzi wa kina kuhusu changamoto hiyo na kuziagiza taasisi kufanya uchambuzi wa maeneo mengine yenye matumizi makubwa ya fedha za kigeni.
Kwa upande wake, Katibu Mkuu Wizara ya Nishati, Mha. Felchesmi Mramba akitoa majumuisho kwa kamati amesema kuwa miongoni mwa hatua ambazo zimechukuliwa kwa ajili ya kuboresha hali ya upatikanaji wa mafuta ni pamoja na kuanza kutumia eneo la kushushia mafuta laTIPER ili kupunguza muda wa kushusha mafuta.
Kamati hiyo ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti kupitia kwa Mwenyekiyi wake. Mhe.Daniel Sillo wameipongeza Serikali kwa kuendelea kuimarisha hali ya upatikanaji wa mafuta nchini kwa kipindi cha kuanzia mwezi Julai, 2023 hadi Sasa na kuwatoa hofu wananchi kuhusu kukosekana kwa bidhaa hiyo nchini na kueleza kuwa hatua zilizochukuliwa na Serikali zinaridhisha.
Kikao cha Kamati ya Bunge ya Bajeti kilihudhuriwa pia na wakuu wa taasisi kutoka EWURA, PBPA, BOT na wadau mbalimbali kutoka Sekta ya Mafuta na Fedha.