Waziri wa nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira Dkt. Seleman Jafo amesema athari zinazotokea za kimazingira ikiwemo hali ya kukosekana kwa umeme ni kutokana na athari za mabadiliko ya tabia na kupelekea kuyumba kwa uchumi.
Jafo amesema hayo alipomwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassa katika uzinduzi wa Jukwaa la ‘Green Samia’ lililoandaliwa na Ofisi ya Rais lengo ni kuwakutanisha vijana kutoka Tanzania bara na Visiwani ili kujadili mabadiliko ya tabia nchi na athari za kimazingira ngazi ya Taifa na kimataifa kuelekea COP28 ambapo watajadili hatua mbalimbali zinazoweza kuchukuwa dhidi ya mabadiliko ya tabia nchi pamoja na mazingira kwa ujumla.
“leo hii mvua inapokosekana mabwawa ya kufua umeme yanapoteza uwezo wake mwishoni mwa mwaka jana bwawa la Mtera lilipoteza uwezo wake kwasababu maji yalikuwa hayatoshi mnaona sasa umeme unapokosekana maana yake uchumi haufanyi vizuri viwanda vitashindwa kufanyakazi vizuri” Dkt. Seleman Jafo
Kwa upande wake Dkt. Richard Muyungi mshauri wa Raisi kuhusu masuala ya mabadiliko ya tabia nchi na mazingia ambaye pia ni mlezi wa jukwaa hilo amesema Tanzania inakuwa miongoni mwa nchi za Kwanza kuanzisha jukaa hilo kwa vijana baada ya kikao cha mwaka 2021 jijini Glasgow kilicholenga kuwachagiza vijana kushiriki vyema katika masuala ya mabadiliko ya Tabia nchi.
Akizungumza kwa niaba ya Vijana wakuoshiriki katika uzinduzi wa Jukwaa hili Laurel Kivuyo Mratibu wa Jukwaa la Green Samia Youth For Climate Action Tanzania amesema vijana Zaidi ya 100 kutoka Zanzibar na Mikoa mbalimbali ya Tanzania bara wameshiriki na lengo ni kupeleka ujumbe kwa vijana wengine nchini.
Kupitia jukwaa hilo Vijana wamepata fursa ya kujifunza na kushiriki kikamilifu kwenye ajenda ya mabadiliko ya tabia nchi kitaifa na kimataifa,diplomasia ya mabadiliko ya tabia nchi, Uhusiano kati ya uwekezaji na uchumi na mabadiliko ya tabia nchi, mfumo na namna mikutano inavyoendeshwa katika mikutano mikubwa ikiwemo mkutano wa COP28 unaotarajiwa kufanyika Dubai mwishoni mwa mwezi Novemba mwaka 2023.