Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi wa Kipalestina limesema kuwa takriban wafanyakazi 17 wameuawa hadi sasa katika mzozo unaoendelea Israel na Hamas. Ilisema kwamba idadi ya vifo inaweza kuongezeka.
“Hadi sasa, wenzetu 17 wamethibitishwa kuuawa katika vita hivi vikali. Cha kusikitisha sana, huenda idadi halisi ikaongezeka,” UNRWA ilisema katika taarifa yake.
Wakati huohuo, watawala wa Hamas wa Gaza waliwaachilia huru Wamarekani wawili siku ya Ijumaa kati ya mateka 200 waliowateka nyara katika mashambulizi ya kikatili ya Oktoba 7 nchini Israel na kuashiria kuwa zaidi wanaweza kufuata.
Hakuna maelezo yoyote yaliyotolewa kuhusu hali yao, lakini Rais wa Marekani Joe Biden alisema “amefurahishwa sana” na habari hizo. Biden alizungumza kwa simu na wanawake hao wawili baada ya kuachiliwa.