Zaidi ya kuku 45,000 wamechinjwa, kuchomwa moto na kuzikwa kusini mwa Msumbiji. Kulingana na maafisa, hatua hiyo inalenga kuzuia kuenea kwa homa ya ndege.
Kuku hao walikuwa wameagizwa kutoka nchi jirani ya Afrika Kusini, ambayo imekumbwa na mlipuko wa ugonjwa huo.
Mlipuko huo sasa umeenea hadi katika wilaya ya Morrumbene nchini Msumbiji katika jimbo la kusini la Inhambane.
Wakati mamlaka zinajaribu kudhibiti ugonjwa huo, kuna hofu kwamba unaweza kuenea katika maeneo mengine ya nchi.
Homa ya ndege ni ugonjwa wa kuambukiza wa kuku na ndege wa mwitu.
Inaweza kuenea kwa makundi yote ya ndege ndani ya muda wa siku chache, kupitia kinyesi cha ndege na mate, au kupitia chakula na maji yaliyochafuliwa.
Nchini Msumbiji, mlipuko huo umesababisha uhaba wa mayai na kuku, na kupanda kwa kasi kwa bei katika siku za hivi karibuni hasa katika mji mkuu Maputo.
Kuku 45,000 walioteketezwa walikuwa wamegusana na kuku walioambukizwa na mafua ya ndege nchini Afrika Kusini, alisema Mkurugenzi wa Kitaifa wa Maendeleo ya Mifugo wa Msumbiji Américo da Conceição.
Afrika Kusini imekuwa ikikabiliana na mlipuko mbaya zaidi wa mafua ya ndege, na kuwalazimu wafugaji wa kuku kuua kuku milioni saba wanaotaga mayai, ambayo ni sawa na 20-30% ya hifadhi nzima ya nchi hiyo, kulingana na Chama cha Kuku cha Afrika Kusini.
Mlipuko huo pia umesababisha uhaba wa usambazaji wa mayai na nyama ya kuku nchini.