Mahakama ya Pakistan imemfungulia mashtaka Imran Khan kwa kuvujisha siri za serikali, kulingana na ripoti. Shtaka hilo linaongeza mzozo mkubwa wa kisheria ambao waziri mkuu huyo wa zamani amekutana nao tangu kuondolewa madarakani Aprili 2022.
“Amefunguliwa mashtaka leo na shtaka hilo lilisomwa wazi,” alisema Shah Khawar wa Shirika la Upelelezi la Shirikisho nje ya Jela ya Adiala huko Islamabad, ambapo Khan amefungwa, kituo cha utangazaji cha Pakistani Geo TV kiliripoti Jumatatu.
Naibu wa zamani wa Khan, Shah Mahmood Qureshi, pia ameshtakiwa katika kesi ya siri za serikali.
Msemaji wa chama cha Khan cha Pakistan Tehreek-e Insaf (PTI) alisema watu hao walishtakiwa chini ya Sheria ya Siri Rasmi ya enzi ya ukoloni katika kesi ya siri, na kuongeza kwamba uamuzi huo “utapingwa”.
Kupitia ripoti za Aljazeera Khan, ambaye aliiongoza Pakistan kuanzia Agosti 2018 hadi Aprili 2022, anashtakiwa kwa kuvujisha barua ya kidiplomasia kati ya Washington na Islamabad ambayo anasema inaashiria jukumu la Marekani katika kumshinikiza kuondoka madarakani.
Marekani na Pakistan zimekanusha madai hayo.