Mkuu wa Wilaya ya Same Kasilda Mgeni amesema uamuzi wa Serikali kujenga chuo cha mafunzo ya ufundi stadi VETA katika Wilaya hiyo utasaidia kuondoa changamoto ya muda mrefu baadhi ya wakazi wa wilaya hiyo hususani vijana kujiingiza katika biashara haramu ya Dawa za kulevya kwa kulima, kusafirisha na kuuza Mirungi.
Ameyasema hayo alipotembelea eneo kunako tekelezwa mradi huo, ujenzi wa Chuo cha VETA Katika kata ya Makanya tarafa ya Chome-Suji, ujenzi uliopangwa kugharimu kiasi cha shilingi Bilioni 1.4 kwa awamu ya kwanza na tayari kiasi cha shilingi Milioni 228 kimekwisha tolewa na tayari ujenzi umekwisha anza tangu Augost mwaka huu 2023.
“Kipekee nimshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe.Dkt.Samia Suluhu Hassani kwa kuona umuhimu wa kujenga Chuo hiki hapa wilaya ya Same kwani kitakua mkombozi kwa vijana wetu ambao wapo mitaani, watajiunga kupata mafunzo yatakayo wasaidia kujiajiri wenyewe na kupunguza wimbi la vijana wasio na ajira ambao wengi wao ndio wamekimbilia kwenye biashara haramu ya Mirungi”.Alisema mkuu huyo wa Wilaya ya Same.
Mkuu huyo wa wilaya amesisitiza ujenzi huo kufanyika kwa haraka na katika viwango na ubora unaokubalika pia kuzingata taratibu zote ikiwemo kwenye manunuzi na utunzwaji wa nyaraka zote muhimu zinazo husiana na ujenzi wa mradi huo.
Kwa upande wake mkuu wa chuo cha Maendeleo ya wananchi (FDC) Same Peter John Maongezi amesema mradi huo kwa awamu ya kwanza unatarajiwa kukamilika ifikapo mwezi Mei 2024, ikihusisha ujenzi wa karakana ya Umeme na Maji,Karakana ya Uselemala na Uashi, karakana ya Upishi na Ushonaji, Vyumba viwili vya Madarasa vyenye ofisi mbili, jengo la utawala , Nyumba ya mkuu wa chuo na kibanda cha Mlinzi kwa Gharama ya shilingi Bilioni 1.4.
Mradi huo unaifanya wilaya ya Same kuwa miongoni mwa wilaya 63 hapa nchini zinazotkeleza ujenzi wa Vyuo vya Ufundi stadi ikiwa ni mpango wa serikali kupitia wizara ya Elimu Sayansi na Teknolojia kuhakikisha kila wilaya inakua na chuo cha Ufundi stadi.