Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron alifika Tel Aviv siku ya Jumanne kueleza “mshikamano kamili” wa nchi yake na Israel baada ya mashambulizi ya Oktoba 7 ya Hamas ambayo yamesababisha hasara kubwa na mgogoro wa kibinadamu.
Macron alikutana na Rais Isaac Herzog mjini Jerusalem baada ya kukutana na familia za wahanga wa Ufaransa alipowasili katika uwanja wa ndege wa Ben Gurion mjini Tel Aviv.
“Ufaransa itasimama kwa mshikamano na Israel katika mapambano yake dhidi ya ugaidi,” Macron alisema alipokutana na mwenzake wa Israel mjini Jerusalem.
“Kilichotokea hakitasahaulika,” Macron alisema, akizungumzia shambulio dhidi ya Israel ambapo Hamas iliua zaidi ya watu 1,400, kati yao 30 walikuwa raia wa Ufaransa. “Niko hapa kueleza mshikamano wetu.”
Kutokana na mashambulizi ya anga ya Israel ya kulipiza kisasi na mashambulizi ya mabomu, zaidi ya Wapalestina 5,000 wakiwemo watoto zaidi ya 2,000 wameuawa shahidi huko Gaza na zaidi ya Wapalestina 15,000 wamejeruhiwa, kulingana na wizara ya afya ya Gaza.
Zaidi ya hayo, matukio ya kutisha huko Gaza yamesababisha zaidi ya Wapalestina milioni moja kuyahama makazi yao.
Macron pia alikutana na Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu.