Siku ya 3 ya michuano ya kombe la dunia inayofanyika nchini Brazil ilishuhudia matumizi ya ‘goal line technology’ kwa mara ya kwanza kwenye soka.
Timu ya taifa ya Ufaransa ndio imekuwa ya kwanza kupata faida ya matumizi ya Teknolojia ya kisasa kuzuia ubishi kuhusu magoli.
Shambulizi la Karim Benzema katika lango la Honduras kunako dakika ya 48 ya kipindi cha pili lilileta kizazaa baada ya mpira kuvuka mstari wa goli kidogo na kipa wa Honduras Noel Valladares akaurudisha uwanjani akitaka kuupiga kama ‘goal kick’ lakini mwamuzi kutoka Brazil Sandro Meira Ricci akapuliza kipenga na kuashiria bao kutokana na mtikiso kwenye saa yake inayoambatana na teknolojia hiyo ya kisasa ya goal line.
Mashabiki na wachezaji wa Honduras waliokuwa ndani ya uwanja wa Porto Alegre walijaribu kupinga kauli ya refarii huyo lakini wapi alihakiki bao hilo la pili kwa Ufaransa .
Honduras ilikuwa tayari imempoteza mchezaji wao Palacios mwisho wa kipindi cha kwanza alipoonyeshwa kadi ya pili ya manjano
Teknolojia hiyo inayotumika kwa mara ya kwanza inajumuisha kamera 14 za kisasa na zenye uwezo mkubwa wa kurekodi picha na sauti kwa kasi mno kufuatana na kasi ya mpira.
Kamera hizo zinauwezo wa kuchukua picha kwa kasi mno (saba kwenye kila lango), katika paa za nyanja zote 12.
Mchezo huo uliopigwa jana majira ya saa nne usiku uliisha kwa Ufaransa kushinda 3-0, Benzema akifunga mawili na lingine likiwa zawadi ya goal line technology.