Takriban raia ishirini waliuawa Jumatatu usiku mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo katika shambulio lililohusishwa na waasi wa ADF, wanaohusishwa na kundi la Islamic State, duru za ndani zilisema.
Shambulio hilo limetokea kwenye viunga vya Oicha, mji ulioko katika eneo la Beni kaskazini mwa mkoa wa Kivu Kaskazini.
“Hadi sasa tuna miili 20,” Nicolas Kikuku, meya wa mji huo, aliambia AFP kwa njia ya simu mapema leo asubuhi.
“Tumeweka miili 26 katika chumba cha kuhifadhia maiti”, alisema Darius Syaira, ripota wa mashirika ya kiraia katika eneo la Beni. Kulingana naye, waathiriwa walikuwa watoto 12 na watu wazima 14, ambao wengi wao waliuawa kwa visu.
Hapo awali waasi wa Uganda waliokuwa na Waislamu wengi, ADF (Allied Democratic Forces) wamekuwepo mashariki mwa DRC tangu miaka ya 1990, ambako wanashutumiwa kwa mauaji ya maelfu ya raia.
Nchini Uganda, mamlaka inawashutumu kwa kuua watu watatu, wakiwemo watalii wawili wa kigeni, tarehe 17 Oktoba katika Mbuga ya Malkia Elizabeth.