Tangu shambulio la Hamas tarehe 7 Oktoba, watoto wapatao 2,000 wameuawa katika mashambulizi ya kulipiza kisasi ya anga ya Israel huko Gaza, kulingana na Save the Children.
Akizungumza na Sky News, mkurugenzi wa nchi wa shirika hilo katika maeneo ya Palestina yanayokaliwa kwa mabavu, Jason Lee, alisema mtoto mmoja aliuawa kila baada ya dakika 13.
“Tuko ukingoni mwa janga la kibinadamu. Ni muhimu kuwe na usitishaji mapigano,” alisema.
“Mahitaji ya watoto yanaongezeka na inazidi kuwa ya kukata tamaa kila siku.”
Alieleza jinsi wafanyakazi wa misaada walivyokuwa wakijaribu sana kuingia katika eneo hilo ili kusaidia na baadhi ya wafanyakazi tayari walikuwa wamepoteza makazi yao, na wanafamilia.
“Moja ya shule za kusini ina watu 23,000 na bafu 16 tu. Hakuna chakula, hakuna maji na wafanyikazi wangu wako katika hali hiyo hiyo,” alisema.
“Lazima turuhusiwe kuingia. Muda unakwenda.”
Msaada mdogo umeanza kuingia katika Ukanda wa Gaza uliozingirwa kutoka Misri, lakini usambazaji wa chakula, maji, madawa na mafuta umekuwa ukipungua sana.