George Weah na Joseph Boakai watachuana katika duru ya pili iliyo karibu sana, kulingana na matokeo ya mwisho yaliyotangazwa na tume ya uchaguzi siku ya Jumanne.
Takriban kura 7,000 zinawatenganisha wawili hao. George Weah alipata 43.83% ya kura na Joseph Boakai, 43.44% wakati wa duru ya kwanza ya uchaguzi wa urais nchini Liberia.
Matokeo haya yanathibitisha mwelekeo uliotolewa na matokeo ya muda katika wiki iliyopita. Ni matokeo tu kutoka kwa vituo vichache vya kupigia kura katika kaunti za Nimba, Sinoe, na Montserrado yaliyokuwa yanasubiriwa, kwani wapiga kura katika maeneo hayo walilazimika kupiga kura tena.
Hakuna hata mmoja kati ya wagombea wawili wakuu aliyeweza kukusanya idadi ya kura zinazohitajika ili kupata wingi kamili. Kinyang’anyiro hicho sasa kiko wazi kurejesha kura za wagombea walioondolewa katika duru ya kwanza.
Kati ya wagombea urais 18wanaosalia, hakuna anayezidisha 3% ya kura. Mgombea wa nafasi ya tatu, Edward Appleton, yuko nyuma sana kwa wapinzani wote wawili. Alipata 2.2% ya kura.
Zimesalia wiki tatu kabla ya duru ya pili inayotarajiwa kufanyika Novemba 14. Wakati huu, kila mmoja wa wagombea atalazimika kuwashawishi wapiga kura wa wagombea wadogo.