Mkuu wa Misaada ya Kibinadamu na Misaada ya Dharura ya Umoja wa Mataifa Martin Griffiths amesema vita vya nusu mwaka vimeitumbukiza Sudan katika “mojawapo ya jinamizi mbaya zaidi la kibinadamu katika historia ya hivi karibuni.”
Wakati mapigano yakiendelea kati ya Jeshi la Sudan (SAF) na kundi la wanamgambo wa Rapid Support Forces (RSF) la Sudan, hadi watu 9,000 wameuawa na zaidi ya watu milioni 5.6 wamelazimika kuyahama makazi yao ndani na nje ya mipaka ya nchi.
“Kwa muda wa miezi sita, raia – hasa katika Khartoum, Darfur na Kordofan – hawajapata nafuu kutokana na umwagaji damu na ugaidi,” Griffiths alisema. “Ripoti za kutisha za ubakaji na unyanyasaji wa kijinsia zinaendelea kuibuka, na mapigano yanazidi kutokea katika misingi ya kikabila, hasa katika Darfur. Hili haliwezi kuendelea.”
Wakati huo huo, Marekani imetoa wito kwa mashambulizi ya makombora katika vitongoji vya kiraia kukomeshwa mara moja, ikisema “Hakuna suluhu la kijeshi linalokubalika kwa mzozo huu – ‘ushindi’ wa pande zote mbili ungesababisha adha isiyovumilika kwa watu wa Sudan na taifa lao.”
Mapigano yalizuka nchini Sudan Aprili 15, kilele cha mvutano wa wiki kadhaa unaohusishwa na mpango wa mpito kuelekea utawala wa kiraia.
Jenerali Abdel-Fattah Burhan, kamanda wa Vikosi vya Wanajeshi vya Sudan na Jenerali Mohammed Hamdan Dagalo mkuu wa Vikosi vya Msaada wa Haraka waliokuwa washirika ambao kwa pamoja walipanga mapinduzi ya kijeshi mwaka 2021 — sasa wanashiriki katika mapambano makali ya madaraka.