Mahakama nchini Nigeria imemhukumu mkurugenzi wa matibabu kifungo cha maisha jela kwa kumbaka mpwa wa mke wake.
Dkt Olufemi Olaleye anaripotiwa kumdhulumu msichana huyo kingono kwa zaidi ya mwaka mmoja hadi mkewe alipojua na kuwaarifu polisi, mwendesha mashtaka alisema.
Olaleye alifikishwa mahakamani Novemba mwaka jana akikabiliwa na mashtaka mawili ya ubakaji kati ya Desemba 2019 na Julai 2022, msichana huyo alipoenda kuishi na familia yao.
Wakati wa kesi hiyo, mke wa daktari huyo, Aderemi Olaleye, alisema aligundua unyanyasaji huo baada ya msichana huyo kumwambia shangazi yake na dereva wa familia hiyo.
Msichana huyo, ambaye kwa sasa ana umri wa miaka 18, alisema daktari huyo alikuwa akilala naye na alitoa vitisho vya kuuawa iwapo angemwambia mtu yeyote.
Pia alishtakiwa kwa kumlazimisha kutazama ponografia.
Mashahidi sita – msichana, mke wa mshtakiwa, daktari, mtaalamu wa malezi ya watoto na maafisa wawili wa polisi waliohusika katika uchunguzi – walitoa ushahidi katika kesi hiyo.
akitoa hukumu siku ya Jumanne, Hakimu Rahman Oshodi alisema ushahidi uliowasilishwa mbele ya mahakama “unamhusisha sana” mshtakiwa.
Kulingana na hakimu, maungamo ya awali ya Olaleye kwa polisi yalithibitisha kwamba alitenda makosa hayo.
Katika ombi lake la kuhurumiwa, wakili wa daktari huyo, Adebisi Oridate, aliomba serikali kutambua huduma za Olaleye kama daktari wa saratani na kwamba alikuwa mkosaji wa mara ya kwanza.
Lakini hakimu alitupilia mbali ombi hilo na kusema kwamba Olaleye lazima afungwe gerezani kwa muda mrefu kama dhibitisho kwamba mfumo wa haki wa Nigeria ulipuuza unyanyasaji wa kingono.
Pia aliamuru jina la daktari kuongezwa kwenye sajili ya wahalifu wa ngono ya Jimbo la Lagos.