Serikali ya Kenya imewasilisha rasmi kwenye bunge la nchi hiyo ombi la kutaka idhini ya kuwapeleka askari polisi 1,000 nchini Haiti kupambana na magenge ya wahalifu.
Kwenye taarifa iliyowasilishwa bungeni jana alasiri, Waziri wa Usalama wa Ndani nchini humo Kithure Kindiki amelitaka Bunge kukubali ombi la Baraza la Kitaifa la Ushauri kuhusu Usalama (NSAC) la kupeleka askari hao nchini Haiti kuanzia Januari 2024.
Amesema askari Polisi hao watashirikiana na vikosi vya usalama kutoka mataifa mengine kusaidiana na jumla ya polisi 10,000 wa Haiti kupambana na wahalifu hao ambao wamevuruga uthabiti katika nchi hiyo.
Haiti imeshuhudia machafuko yaliyosababishwa na magenge ya wahalifu tangu kuuawa kwa aliyekuwa Rais wa nchi hiyo Jovenel Moise mwezi Julai, 2021.