Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Russia amesema: Katika hali ya sasa, usitishaji vita ndiyo njia rahisi na ya wazi zaidi ya kuzuia mauaji ya watoto wa Gaza.
Kwa mujibu wa shirika la habari la TASS, Maria Zakharova ameashiria jinsi Wamagharibi wasivyojali kuhusiana na mauaji ya umati yanayofanyika Ukanda wa Gaza na kusisitiza kuwa:
“Baadhi ya mirengo ya kisiasa katika nchi za Magharibi imethibitisha kwamba, hata baada ya kuchapishwa ripoti zinazoeleza kwamba maelfu ya watoto wameuliwa kikatili huko Gaza, haitaki kuwasilisha rasimu katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kwa ajili ya kuanzisha usitishaji vita na kutatua mzozo wa Israel na Palestina”.
Hadi sasa, Russia imewasilisha rasimu mbili katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kwa ajili ya usitishaji vita huko Gaza, lakini rasimu ya kwanza imepingwa na nchi za Magharibi zikiongozwa na Marekani.
Kwa mujibu wa ripoti ya Shirika la Kuhudumia Watoto la Umoja wa Mataifa (UNICEF), zaidi ya watoto 2,300 wameuawa katika mashambulizi ya jeshi la Israel Ukanda wa Gaza na zaidi ya wengine 5,300 wamejeruhiwa.