Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) imetangaza Awamu ya Kwanza ya wanafunzi 56,132 wa Shahada ya Kwanza waliopangiwa mikopo yenye thamani ya TZS 159.7 bilioni kwa mwaka wa masomo 2023/2024.
Mkurugenzi Mtendaji wa HESLB Abdul-Razaq Badru amesema kuwa kati ya wanafunzi hao, wa kiume ni 32,264 (57%) na wa kike ni 23,868 (43%) na kuongeza ya kuwa wanafunzi hao wanaweza kuona tarifa za mikopo waliyopangiwa. “Akaunti hizo za SIPA (Student’s Individual Permanent Account) ambazo walitumia kuomba mkopo na ndiyo sehemu muhimu ya kupata taarifa kuhusu ombi la mkopo kwa mwombaji mkopo yeyote,” amesema Badru katika mkutano na wanahabari jijini Dar es salaam.
Kuhusu utaratibu wa kupokea fedha hizo, Badru amesema maafisa wa HESLB watakua katika taasisi za elimu ya juu nchini kuanzia Jumatatu, Oktoba 23, 2023 ili kuratibu usajili wa wanafunzi hao katika mfumo wa malipo. “Kwa wanafunzi wapya, wafike vyuoni wakiwa na namba za akaunti zao benki, namba zao za simu zinazopatikana na watasajiliwa katika mfumo wetu wa malipo wa DiDiS (Digital Disbursement Solution) baada ya kusajiliwa na chuo,”amesema.
Kuhusu kutangazwa kwa orodha ya Awamu ya Pili, Mkurugenzi Badru amesema itatolewa kabla ya Oktoba 27, 2023 baada ya kukamilishwa uchambuzi wa maombi unaoendelea na kuwasisitiza waombaji mikopo kutembelea akaunti zao za SIPA kwa taarifa za maombi yao.
TZS 731 Bilioni zimetengwa kwa wanafunzi wa shahada ya kwanza kwa 2023/2024 Badru amesema Serikali imetenga TZS 731 Bilioni kwa ajili ya wanafunzi 220,376, kati yao, wanafunzi 75,000 watakuwa ni wanufaika wa mwaka wa kwanza wa Shahada ya kwanza na wanafunzi zaidi ya 145,376 ni wanaoendelea na masomo baada ya kufaulu mitihani yao.
Naye Rais wa TAHLISO Maria John Thomas amesema… “Tunamshukuru Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kutusikiliza na kutuwezesha … tarehe 11 Februari, 2023 tuliomba fedha ya kujikimu iongozewe, sasa imeongezwa hadi TZS 10,000 kwa siku… tuliomba wenzetu wa vyuo vya kati wapewe mikopo, nao wameanza kupewa mikopo.”