Ukanda wa Gaza, uliozingirwa tangu Oktoba 7 kwa jumla na mashambulizi ya mabomu ya Israel, unahitaji haraka msaada “muhimu na endelevu”, anaonya mkuu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Wakimbizi wa Kipalestina (UNRWA).
Wakati wa mkutano na waandishi wa habari mjini Jerusalem, Philippe Lazzarini pia amedokeza kuwa shirika lake limethibitisha vifo vya wafanyakazi wake 57 katika ardhi ndogo ya Palestina tangu kuanza kwa vita kati ya Israel na kundi la wanamgambo wa Kiislamu la Hamas kutoka Palestina.
“Huduma za kimsingi zinaporomoka, vifaa vya dawa, chakula na maji vinaisha, mifereji ya maji taka inaanza kufurika katika mitaa ya Gaza,” ameeleza mkuu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi wa Kipalestina (UNRWA), Philippe Lazzarini.
Misafara ya misaada ambayo imeingia katika ardhi ya Palestina tangu Oktoba 21 kwa kiasi kikubwa haitoshi kukidhi mahitaji ya watu, afisa huyo amesema. “Mfumo wa sasa unaelekea kushindwa. Tunachohitaji ni msaada mkubwa na unaoendelea, tunahitaji usitishaji mapigano wa kibinadamu ili misaada hii iweze kuwafikia wanaoihitaji,” amesema.