Uchunguzi ulianza Alhamisi kuhusu moto wa jengo la ghorofa ulioua watu 76 nchini Afrika Kusini mwezi Agosti na kuweka wazi matatizo makubwa ya umaskini na kutelekezwa katika sehemu za jiji hilo tajiri zaidi barani Afrika.
Moto huo wa usiku ulikumba jengo la orofa tano katika wilaya ya Marshalltown ya Johannesburg, na kuwaweka mtego mamia ya watu waliokuwa wakiishi humo katika hali mbaya ya msongamano.
Jengo hilo liliaminika kuwa mojawapo ya yale yanayojulikana kama majengo “yaliyotekwa nyara” huko Johannesburg. Mamlaka inashuku ilikuwa imechukuliwa na wamiliki wa nyumba kinyume cha sheria, ambao walikuwa wanakodisha nafasi kwa Waafrika Kusini maskini na wahamiaji wa kigeni waliokuwa wakitafuta mahali pa kuishi.
Kaimu mkuu wa Huduma za Dharura za Johannesburg Rapulane Monageng alitoa ushuhuda wa kwanza wa uchunguzi huo na kusema kuwa wazima moto hawakupata vifaa vya kuzimia moto popote katika jengo hilo.
Wote walikuwa wametolewa nje ya kuta, alisema. Bomba kubwa la kuzimia moto pia lilikuwa limetolewa na bomba la maji lililokuwa likisambaza lilibadilishwa kwa ajili ya “matumizi ya nyumbani,” alishuhudia.