Ripoti zinasema kuwa katika hali ya kusikitisha, familia zinazoepuka ghasia na machafuko nchini Sudan zinaendelea kuwasili katika maeneo ya mbali ya kaskazini mwa Sudan Kusini.
Raia wanaokimbia makazi yao huko Sudan wanatafuta hifadhi katika maeneo ambayo mashirika ya misaada ya kibinadamu yanapambana na changamoto kubwa ya kusambaza misaada ya dharura.
Imeelezwa kuwa hali hii inachangiwa zaidi na msimu wa mvua na ukosefu mkubwa wa fedha za wafadhili, jambo ambalo linakwamisha juhudi za kuwahamisha kutoka katika maeneo ya mpakani.
Hii imezidisha hali mbaya ya kibinadamu katika kituo cha kuwapokea wakimbizi kwa muda ambacho tayari kimejaa idadi kubwa ya watu katika mji wa mpakani wa Renk.
Tangu kuibuka mapigano huko Sudan mwezi Aprili mwaka huu, yaani katika kipindi cha miezi sita watu wanaokadiriwa milioni 6 wamelazimika kuhama makazi yao na kujaribu kutafuta hifadhi katika nchi jirani ikiwemo huko nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati, Chad, Misri, Ethiopia na Sudan Kusini.