Miaka mitano baada ya kuanza kutekelezwa kwa Sheria ya Uwezeshaji Wazawa (Local Content) mafanikio yameanza kuonekana kuwa lulu kwa Watanzania huku fursa za ajira zikizidi kufunguliwa.
Sheria hiyo ya mwaka 2018 iliyofanyiwa marekebisho mwaka 2019 inalenga kutoa fursa kwa Watanzania kushiriki kikamilifu katika uchumi wa madini.
Mafanikio hayo yameelezwa katika Maonesho ya Sita ya Teknolojia ya Madini Geita wakati wa kongamano la wadau wa sekta ya madini kujadili fursa za uwekezaji kupitia sheria hiyo lililofanyika katika Maonesho ya Sita ya Kimataifa ya Teknolojia ya Madini yanayofanyika kuanzia Septemba 20 hadi Oktoba 1, 2023 katika viwanja vya EPZA Bombambili mkoani Geita.
Kamishna wa ‘Local Content’, Janeth Lukeshingo anasema ajira zimeongezeka, manunuzi ya bidhaa na huduma kwa Watanzania, ushirikishwaji na uhaulishaji wa teknolojia na utafiti, maendeleo na kuongezeka kwa uelewa kuhusu ushirikishwaji wa Watanzania katika seta ya madini.
Mratibu wa Local Content katika Kampuni ya Geita Gold Mining Limited (GGML) Riwald Tenga, anasema wanatekeleza sheria hiyo kwa asilimia 90.
“Tunafuata masharti yote katika manunuzi na katika utoaji ajira, yote tunayofanya kwenye Local Content tuko kati ya asilimia 60 mpaka 90,” anasema Tenga.
AngloGold Ashanti ambayo ni kampuni mama ya GGML, hivi karibu ilitoa kandarasi ya usafirishaji wa mafuta, yenye thamani ya takriban Sh bilioni 25 kwa mwaka kwa wakandarasi wawili wa Tanzania.
Miongoni mwa makampuni ya ndani yaliyonufaika ni pamoja na Blue Coast Investment Limited, kampuni ya Geita inayojishughulisha na usafiri na usafirishaji.
WAWEKEZAJI WAZAWA
Mkurugenzi Mtendaji wa Blue Coast, Ndahilo Athanas anasema wameanza kufanya biashara na GGML tangu mwaka 2021.
“Tunaishukuru Serikali kwa kuona umuhimu wa sheria hii na kuipitisha, lakini tunamshukuru zaidi Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kusimamia utekelezaji wa sheria hii.
“GGML wana mchango mkubwa wa kutufikisha hapa tulipo, wamekuwa chachu ya sisi kufikia viwango vya ubora. Wametupatia elimu ya kutosha juu ya umuhimu wa ubora na namna ya kuendelea kufanya biashara endelevu,” anasema Athanas.
Anasema wanaendesha shughuli zao kupitia viwango vya kitaifa na kimataifa ambapo wana cheti cha usalama kazini, cheti cha ubora wa kazi na sasa wanaendelea na usajili wa ubora katika usimamizi wa mazingira.
Kwa mujibu wa mkurugenzi huyo, kampuni hiyo imeajiri zaidi ya wafanyakazi 400 kwenye ajira rasmi na zisizo rasmi kwa wakazi wa Geita na maeneo mengine yanayozunguka mkoa huo na kufanya idadi kufikia 580 kutoka 220 wa mwaka 2021.
Aidha, anasema wamejikita kutoa elimu kazini ili kuwajengea uwezo vijana kabla ya kuwapa ajira rasmi hasa wahitimu wa vyuo vikuu.
“Mpaka sasa vijana 50 wameajiriwa kupitia utaratibu huu katika nyanja mbalimbali kama uhasibu, maofisa ugavi, mafundi magari, maofisa uendeshaji na nyingine,” anasema.
Mkurugenzi huyo anasema pia wamepata tuzo ya mlipakodi bora kwa Mkoa wa Geita na kwamba kupitia fursa ya Local Content kampuni hiyo imekua na sasa imehamishiwa kwenye kundi la walipakodi wakubwa.