Rais wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan amempongeza Spika wa Bunge la Tanzania, Dkt. Tulia Ackson kwa kuchaguliwa kuwa Rais wa Umoja wa Mabunge Duniani (IPU) katika uchaguzi uliofanyika leo Jijini Luanda nchini Angola.
Rais Samia amesema “Ushindi huu ni ushuhuda wa kazi kubwa unayoendelea kuifanya na imani Wajumbe waliyonayo juu yako na Nchi yetu, kuchaguliwa kwako pia ni matokeo ya miaka mingi ya kazi, weledi na kujituma katika utumishi wa umma, mfano bora kwa Watoto wa kike katika Nchi yetu, Afrika na hata nje ya mipaka ya bara letu”
Dkt. Tulia ameshinda Urais huo baada ya kupata kura 172 kati ya kura 303 zilizopigwa na anarithi mikoba ya Rais aliyemaliza muda wake, Duarte Pacheco kutoka Ureno, Wagombea wengine walioshiriki Uchaguzi huo ni Catherine Hara kutoka Malawi kura 61, Adji Diarra kutoka Senego kura 51 na Marwa Hagi kutoka Somalia kura 11.
Dkt. Tulia amesema kuwa hii ni nafasi kubwa kwa Tanzania kuonekana zaidi duniani na ameahidi kutangaza amani duniani ikiwemo kuziepusha Nchi kujiingiza katika vita.