Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Tulia Ackson, amechaguliwa kuwa Rais wa Umoja wa Mabunge Duniani (IPU) katika uchaguzi uliofanyika leo October 27, 2023 Jijini Luanda nchini Angola.
Dkt. Tulia ameshinda Urais huo baada ya kupata kura 172 kati ya kura 303 zilizopigwa na anarithi mikoba ya Rais aliyemaliza muda wake, Duarte Pacheco kutoka Ureno, Wagombea wengine walioshiriki Uchaguzi huo ni Catherine Hara kutoka Malawi kura 61, Adji Diarra kutoka Senego kura 51 na Marwa Hagi kutoka Somalia kura 11.
Dkt. Tulia amesema kuwa hii ni nafasi kubwa kwa Tanzania kuonekana zaidi duniani na ameahidi kutangaza amani duniani ikiwemo kuziepusha Nchi kujiingiza katika vita.
Kwa upande wake Naibu Spika wa Bunge la Tanzania Mussa Zungu amempongeza Dkt. Tulia kwa hatua hiyo na kumtakia mafanikio mema katika majukumu yake hayo mapya.