Rais William Ruto wa Kenya amesema kuwa, nchi yake itaondoa masharti ya kuchukua visa kwa raia wote wa nchi za Afrika ifikapo mwishoni mwa mwaka huu wa 2023 kwa lengo la kuimarisha biashara na nchi za Afrika.
Rais Ruto amesema hayo huko Brazzaville, mji mkuu wa Jamhuri ya Kongo kwenye kikao cha mabonde matatu makubwa ya misitu duniani duniani ambayo yanajulikana kwa majina ya Amazon, Kongo na Borneo-Mekong.
Amesema: “Mwishoni mwa mwaka huu, hakuna Mwafrika atakayehitaji visa kuingia Kenya. Wakati umefika wa kuelewa umuhimu wa kufanya biashara kati yetu.”
Vilevile amezungumzia kiwango cha chini cha biashara ya ndani ya Afrika na akahimiza kupunguzwa ushuru wa forodha ndani ya bara la Afrika ili kuharakisha utekelezaji wa Eneo Huru la Biashara la Bara la Afrika.
Katika sehemu nyingine ya hotuba yake, Rais huyo wa Kenya amesema: “Imefika wakati tutambue umuhimu wa kufanya biashara kati yetu na kuruhusu bidhaa, huduma, watu na mawazo kutembea kwa uhuru katika bara zima.”
Ameongeza kuwa, biashara kati ya nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) imekua kwa kiasi kikubwa kutokana na kuondolewa viza na ushuru.
Aidha Rais Ruto amesema kuwa, kutambua na kutoa motisha kwa nchi zilizoko kwenye mabonde ya misitu ya tropiki kwa ajili ya kulinda misitu hiyo ni hatua nzuri ya kulinda hali ya hewa.