Shirika la Mpango wa Chakula Duniani (WFP) limetangaza kuwa, linahitaji dola za Kimarekani milioni 351 katika ufadhili jumla kwenye shughuli zote ili kuongeza msaada wa kibinadamu kwa miezi sita ijayo nchini Somalia.
Madhara ya miongo kadhaa ya migogoro ya silaha, mvua zisizo za kawaida, umaskini na wakimbizi wa ndani vimesababisha mamilioni ya watu nchini Somalia kuelekea kwenye njaa kali na uhaba wa chakula.
Kwa mujibu wa shirika hilo la Umoja wa Mataifa, kati ya Oktoba na Desemba, takriban watu milioni 4.3 watakuwa wanakabiliwa na mgogoro mbaya zaidi wa uhaba wa chakula, huku milioni moja wakihitajia misaada ya dharura ya kukabiliana na baa la njaa.
Katika ripoti yake ya hivi karibuni kabisa, WFP imesema kwamba, idadi ya watoto wenye umri wa chini ya miaka mitano wanaokadiriwa kukabiliwa na utapiamlo mkali mwaka 2023 imepungua hadi milioni 1.5, huku watoto 331,000 wakiwa bado wanakabiliwa na utapiamlo unaotishia maisha.
Ripoti hiyo imeongeza kuwa, takriban watu milioni 1.2 wanaoishi katika maeneo ya vijijini, mijini na wakimbizi wa ndani kwenye maeneo ya mafuriko wanakabiliwa na vitisho vya mafuriko kutokana na athari ya pamoja ya El Nino na hali nzuri ya Bahari ya Hindi wakati wa msimu wa mvua wa Deyr unaoanzia mwezi Oktoba hadi Desemba.