Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Adam Malima amesema jitihada za haraka zinahitajika ili kuuwezesha Mkoa huo, kuzalisha maji kwa wingi ili kuboresha huduma ya maji kwa watumiaji kwa kuanzisha mifumo ya uvunaji maji ya ziada yanayotiririka na chini ya ardhi.
Akizungumza katika kikao cha wadau na wasambazaji wa huduma za maji mkoani Morogoro, ambao wamekutana kwa pamoja kujadili na kutafuta ufumbuzi wa suluhisho la kudumu katika kuimarisha huduma ya uzalishaji wa maji, amesema pamoja na serikali kuwekeza fedha nyingi katika miradi ya maji mkoani humo bado kiwango cha huduma ya maji hakikidhi mahitaji ya watumiaji.
Amesema kunahitajika kuanzishwa mkakati wa kuanza kuvuna maji katika mito kwa kujenga mabwawa ya maji, pamoja na kudhibiti uharibifu wa mazingira ambapo tayari miche ya miti ya mikarafuu imeanza kupandwa katika Halmashauri ya Morogoro.
Rc Malima amesema anatambua mchango wa mamlaka za utoaji huduma ya maji mkoani humo lakini bado jitihada za makusudi zinahitajika ili kuhakikisha huduma hiyo inaimalirika .
Kwa upande wake Kaimu Meneja RUWASA Mkoa wa Morogoro Mhandisi Sospeter Lutonja akizungumza katika kikao hicho ameeleza jitahada mbalimbali zinazofanyika katika kusogeza huduma ya maji kwa jamii ambapo matarajio yao ni kufikia asilimia 84.46 ifikapo Juni 2024.
Mhandisi Lutonja amesema kwa sasa mamlaka hiyo inatekeleza miradi mbalimbali katika maeneo tofauti mkoani humo lengo kila mwananchi apate huduma hiyo
Naye, Mkurugenzi Mtendaji Bonde la Wami/Ruvu Mhandisi Elbariki Mmasy akaeleza kuwa katika maji yanayozalishwa Lita milioni 218 hutumika kwa ajili ya matumizi ya nyumbani, viwanda Lita milioni 67, shughuli za uchimbaji madini na mazingira lita milioni 87 huku akieleza pia tafiti ambazo zimefanyika na kubaini maeneo yenye maji chini ya ardhi.