Maafisa wa Palestina katika Ukanda wa Ghaza wanasema utawala wa Israel umedondosha karibu tani 20,000 za mabomu ya mauaji katika eneo hilo tokea kuanza vita vyake vya uchokozi dhidi ya wakazi wa ukanda huo.
Katika taarifa yake Jumatatu, Ofisi ya Vyombo vya Habari ya Ukanda wa Ghaza imesema kuwa jeshi katili na vamizi la Israel limedondosha zaidi ya tani 18,000 za milipuko kwenye Ukanda wa Ghaza katika kipindi cha siku 24 zilizopita.
Taarifa hiyo imeongeza kuwa watu 10,000 ama wameuawa au bado hawajulikani walipo kutokana na mashambulizi makali hayo ambayo pia yamesababisha uharibifu mkubwa wa makazi na miundomsingi.
Ofisi hiyo imesema kufikia sasa tani 50 za milipuko zimedondoshwa katika kila kilomita ya ukanda huo.
Kauli hiyo imekuja baada ya ofisi ya vyombo vya habari ya muqawama wa Palestina Hamas huko Ghaza kusema wiki iliyopita kwamba Israel imeshambulia Ghaza kwa zaidi ya tani 12,000 za mabomu. Imeongeza kuwa tani hizo ni sawa na bomu la nyuklia lililotumika huko Hiroshima nchini Japan.
Mapema Jumatatu, Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Umoja wa Kiislamu (OIC) Hussein Brahim Taha alisema katika taarifa kwamba mashambulio ya mara kwa mara ya Israel dhidi ya Ukanda wa Ghaza unaozingirwa na Wazayuni ni jinai za kivita na ukiukaji wa wazi wa sheria za kimataifa.
Ameongeza kuwa mashambulio ya anga ya Israel pia yamepelekea kujeruhiwa raia wasio na hatia, wakiwemo wanawake, watoto, wafanyakazi wa huduma za afya pamoja na waandishi wa habari.