Mamilioni ya Waafghanistan wamemiminika nchini Pakistan katika miongo ya hivi karibuni, wakikimbia mfululizo wa migogoro mikali, ikiwa ni pamoja na takriban 600,000 tangu serikali ya Taliban ichukue mamlaka mnamo Agosti 2021 na kuweka tafsiri yake kali ya sheria za Kiislamu.
Pakistan imesema kufukuzwa nchini humo ni kulinda “usalama” wake baada ya kuongezeka kwa kasi kwa mashambulizi, ambayo serikali inalaumu wanamgambo wanaoendesha harakati zao kutoka Afghanistan.
Wachambuzi wanasema huenda ni mbinu ya kushinikiza kulazimisha serikali ya Taliban kushirikiana katika masuala ya usalama.
Ubalozi wa Afghanistan mjini Islamabad umesema hatua hiyo itaharibu zaidi uhusiano kati ya majirani hao wawili.
Siku ya Alhamisi, zaidi ya watu 100 walizuiliwa katika operesheni moja ya polisi katika mji mkuu wa Karachi siku ya Alhamisi, huku polisi wakiwakamata Waafghanistan 425 huko Quetta, jiji lililo karibu na kivuko cha mpaka cha Chaman.
“Kampeni dhidi ya wahamiaji haramu itaendelea,” Saad Bin Asad, naibu kamishna wa jiji hilo, aliiambia AFP.
Wanasheria na makundi ya kutetea haki za binadamu yameishutumu serikali ya Pakistani kwa kutumia vitisho, unyanyasaji, na kuwekwa kizuizini kuwalazimisha waomba hifadhi wa Afghanistan kuondoka huku Waafghanistan wakiripoti wiki kadhaa za kukamatwa kiholela na unyang’anyi.