Rais wa Umoja wa Falme za Kiarabu amesema kuwa inapanga kuwatibu watoto 1,000 wa Kipalestina kutoka Gaza.
Sheikh Mohamed bin Zayed Al Nahyan hakueleza jinsi watakavyoondoka katika eneo lililozingirwa na kuelekea jimbo la Ghuba, katika maoni yaliyoripotiwa na WAM.
Shirika la habari la serikali lilisema watoto hao wa Kipalestina “watarejea nyumbani” baada ya kupata huduma za matibabu.
Haijabainika mara moja iwapo watoto hao na familia zao wataweza kuhama Gaza chini ya makubaliano yaliyokubaliwa kati ya Hamas, Israel na Misri kuruhusu raia wa kigeni na baadhi ya Wapalestina waliojeruhiwa kutumia kivuko cha Rafah.
Israel imeimarisha mzingiro wake wa Gaza kwa takriban wiki nne, na kuruhusu raia 335 wa kigeni na Wapalestina 76 waliojeruhiwa vibaya kuondoka jana kwa mara ya kwanza tangu tarehe 7 Oktoba.