Wagombea kadhaa wa uchaguzi wa rais katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo wamesema kuwa, kuna haja ya kuweko mazungumzo kabla ya kufanyika uchaguzii ujao wa Rais nchini humo ili kujadili masuala muhimu.
Wagombea hao akiwemo Moise Katumbi wanaitaka Tume ya Uchaguzi ya nchi hiyo CENI kuweka hadharani daftari la orodha ya wapigaji kura.
Katika taarifa ya pamoja wagombea sita wa urais wanakosoa kile wanachoeleza kuwa “ukosefu wa uwazi” katika uendeshaji wa shughuli za uchaguzi.
Moïse Katumbi, Martin Fayulu, Denis Mukwege, Franck Diongo, Josée-Marie Ifoku na Seth Kikuni wana wasiwasi kuhusu kutokuwepo kwa uwazi katika mchakato wa ufadhili wa uchaguzi.
Kadhalika wagombea hao wa kiti cha urais wanataka mashauriano bora kati ya tume ya uchaguzi CENI na wagombeaji wote katika uchaguzi wa urais.