Serikali ya Ujerumani imeahidi kushirikiana na Serikali ya Tanzania kuboresha Makumbusho ya Majimaji ili kuhifadhi kumbukumbu sahihi kwa ajili ya wakati huu na kwa vizazi vijavyo.
Ahadi hiyo imetolewa na Rais wa Jamhuri ya Shirikisho la Ujerumani, Mhe. Dkt. Frank-Walter Steinmeier alipotembelea Makumbusho ya Vita vya Maji Maji Songea Mkoani Ruvuma.
Mhe., Dkt. Steinmeier amesema Ujerumani ipo tayari kufanya uchambuzi na mchakato wa historia ya vita vya Maji Maji kwakuwa kilichotokea zamani hakipaswi kusauhilka na mtu yoyote.
“Ili kuweka kumbukumbu sawa kwa sasa na kwa wakati ujao, Ujerumani tunaahidi kushirikiana na Tanzania kuboresha makumbusho hii,” alisisitiza Mhe. Rais Steinmeier.
Mhe. Dkt. Steinmeier alisema Ujerumani inatamani kufanya uchambuzi na mchakato wa historia ya ‘Vita vya Maji Maji’ na kuongeza kuwa mchakato huo utahusisha vijana, wanafunzi wa shule na vyuo vikuu, wasomi na wataalamu wa hifadhi na sehemu za kumbukumbu.
“Mwaka 2024, Ujerumani inampango wa kufanya maonesho kwa kushirikiana na Makumbusho ya Taifa ya Tanzania, maonesho hayo yatajulikana kwa jina la “Historia ya Tanzania”, alisema Mheshimiwa Steinmeier.
Awali Waziri wa Utamaduni Sanaa na Michezo, Mhe. Dkt. Damas Ndumbaro (Mb.) alisema historia ya Tanzania na Ujerumani ina sura mbili tofauti. Alifafanua kuwa sura ya kwanza ni kuhusu vita waliyopigana babu zetu na sura ya pili ni yale mazuri yaliyofanywa na Serikali ya Ujerumani Kama vile kujenga shule, hospitali na kutoa huduma nyingine za kijamii.