Asamoah Gyan, aliyekuwa staa wa Ligi Kuu ya Uingereza na mchezaji wa timu ya taifa ya Ghana, ameamriwa kumpa mke wake wa zamani nyumba mbili na magari mawili na kiwanja kinachotarajiwa kuwa kituo cha mafuta na hii ni baada ya mahakama kuamua kuwa yeye ndie baba wa watoto watatu waliozaliwa katika ndoa hiyo.
Mahakama iliamuru kuwa nyota huyo wa zamani kumkabidhi Gifty nyumba yake moja iliyoko nchini Uingereza na Accra, nchini Ghana pamoja na magari ya kifahari ya BMW na Infiniti. Kile kilichozua gumzo mitandaoni ni kitendo cha mahakama pia kuamuru mwanamke huyo kupewa kiwanja nchini Ghana kilichotengwa kwaajili ya ujenzi wa kituo cha mafuta. Gyan pia aliambiwa amlipe Gifty cedis 25,000 sawa na £1,730 (Tzs Mil 5.3) kwa mwezi kwa ajili ya malezi ya watoto wake.
Katika kesi iliyokuwa ikiendelea kwa takriban miaka mitano sasa dhidi ya aliyekuwa mke wake aitwae Gifty, Mahakama iliamuru vipimo vya DNA kufanyika baada ya Asamoah Gyan kudai kuwa watoto hao sio wake. Mahakama kuu ya Accra sasa imemtangaza mwenye umri wa miaka 37 kuwa baba wa watoto wa tatu aliyezaa na mwanamke huyo.