Takriban wanamgambo 11, wakiwemo washambuliaji waliowaua watalii wawili na muongoza watalii wao katika Mbuga ya Kitaifa ya Malkia Elizabeth, Mkoa wa Magharibi mwa Uganda mwezi uliopita wameuawa.
Msemaji wa Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Uganda (UPDF) Lt Kanali Deo Akiiki alisema washambuliaji walipigwa risasi Jumanne usiku kwenye Ziwa Edward, karibu na mpaka wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.
UPDF iliripoti kwamba raia wa Uingereza David Barlow na mkewe wa Afrika Kusini Emmaretia Geyer walipigwa risasi na kuuawa kwenye fungate kwenye shambulio la Oktoba 17.
Mwongoza watalii kutoka Uganda Eric Alyai – ambaye ameacha mke na mtoto wa mwaka mmoja – pia aliuawa katika shambulio hilo.
“Mara moja tulianzisha operesheni kubwa ya kuwasaka wanamgambo kutoka Allied Democratic Forces (ADF),” anasema Lt Kanali Deo Akiik.
Kundi la waasi la ADF, lenye uhusiano na Dola la Kiislamu lililoko magharibi mwa Uganda, wengi wao wanaendesha harakati zao katika eneo la mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.
Wapiganaji wake mwezi Juni walivamia shule moja nchini Uganda katika shambulio la kushtukiza, na kuua takriban watoto 41.