Programu hii wa mafunzo itawatambulisha maofisa hao kwenye mapinduzi ya programu ya simu ya mkononi (Mobile App) iliyoandaliwa kupitia jitihada za ushirikiano kati ya Kikosi cha Usalama Barabarani na TBL.
Programu hii bunifu imewekwa ili kuunda upya mazingira ya ukusanyaji, uchanganuzi na utoaji wa taarifa na takwimu za Askari wa Usalama barabarani nchini.
Programu mpya ya simu ya mkononi iliyotengenezwa itachukua jukumu muhimu katika kurahisisha ukusanyaji wa taarifa za Askari wa usalama barabarani, kwa kuruhusu maafisa kuandika na kupakia taarifa za matukio moja kwa moja kwenye seva salama. Hii itawezesha Jeshi kuondokana na mifumo ya sasa, ambapo taarifa hukusanywa katika vituo vya polisi kimoja kimoja, na hatimaye kukusanywa kwa wilaya, mkoa, na, hatimaye, kitaifa.
Manufaa ya mfumo huu mpya ni mengi kwa Jeshi la Polisi Tanzania, watathimini mipango ya barabara, makampuni ya bima na wadau wengine. Kwa ufikiaji wa data ya wakati halisi, mipango na usimamizi wa usalama barabarani utakuwa sahihi na mzuri zaidi. Zaidi ya hayo, madereva pia watafaidika kutokana na kuharakisha kwa madai ya bima, kupunguza muda na utata unaohusishwa na taratibu hizo.
Akizungumza wakati wa uzinduzi wa mafunzo hayo, Mkurugenzi wa Usambazaji wa TBL, Nancy Riwa alisema ni fahari na heshima kubwa kwa TBL kuwa sehemu ya mpango huo muhimu. Alitoa shukrani za kampuni hiyo kwa ushirikiano na msaada walioupata kutoka kwa Jeshi la Polisi Tanzania wakati wote wa utayarishaji wa mfumo huu mpya.
TBL inatambua mchango na busara uliotolewa na Jeshi la Polisi katika kuandaa muundo wa program hii. Mpango huu ni mwendelezo wa ushiriki wa muda mrefu wa TBL katika kusaidia usalama barabarani nchini, na kusisitiza dhamira ya kudumu ya kampuni hiyo kusaidia Polisi wa Usalama Barabarani na wadau wengine.
Katika taarifa yake, Riwa alisema, “Tanzania Breweries Ltd. inajivunia kupewa heshima ya kuwa sehemu ya mpango huu muhimu sana. Tunashukuru kwa ushirikiano na msaada wa Jeshi la Polisi la Tanzania kwa kufanya kazi nasi kuunda hii programu mpya. Tunatambua mchango wao wa busara katika uundaji wa program. Huu ni mwendelezo wa historia ndefu ya ushiriki wetu katika usalama barabarani nchini, na tunapenda kusisitiza tena dhamira yetu ya kuendelea kusaidia Jeshi la Polisi Kikosi cha Usalama Barabarani na wadau wengine kuhakikisha kwamba tunajenga mifumo imara na madhubuti ya usalama barabarani katika nchi hii ili kupunguza ajali na, natumaini siku moja kukomesha vifo vitokanavyo na ajali barabarani zinavyoweza kuzuilika.”