Katibu Mkuu Wizara ya Habari Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mohammed Khamis Abdulla amewataka vijana hususani wanafunzi kuishi maisha ya TEHAMA kwani Dunia ndiko inakoelekea.
Hayo ameyasema Jijini Dar es Salaam katika hafla ya uzinduzi wa kitabu Cha uanzishaji na uratibu wa Klabu za kidijiti ambapo amesema kuanzishwa kwa kitabu hicho ni muongozo wa vijana kupata fursa ya mapinduzi ya kidijiti.
Aidha amezitaka Taasisi za Elimu nchini kuanzisha klabu za kidijiti na zifanye kazi kwa uwazi, uadilifu zikizingatia maadili na faragha kwani ni njia mojawapo ya kufiki jamii na kuwajengea watoto kidijiti katika umri mdogo.
“Kuanzishwa kwa klabu za kidijiti kutasaidia kuchagiza ujuzi na tamaduni za kibunifu kwa wanafunzi na kujenga Taifa la kidijitali ambalo litachangia ufumbuzi wa changamoto na kuwawezesha vijana kuwa wabunifu na wajasiriamali” Amesema Katibu Mohammed.
Ameongeza kuwa kupitia kitabu hicho kitasaidia kuleta dira ya ubunifu katika nchi ambapo sera ya mwaka 2016 ipo kwenye mchakato wa kubadilishwa ambapo itachochea mtaala na kuandaa sera ya kampuni changa ambayo itawasaidia wanafunzi kuwa wadau wakubwa, katika masuala hayo.
Sambamba na hayo amewasisitiza Wanafunzi kujifunza TEHAMA kwani watakuwa bora zàidi na kusaidia taifa kukuza uchumi na mikakati ya kukuza taaluma hiyo na kuziba pengo la taaluma ya kidijiti.
Awali Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania TCRA Dk.Jabir Bakari amesema klabu za kidijiti ni majukwaa ya hiari yanayowakutanisha wanafunzi wa rika moja kupata uelewa na kuhamasishana juu ya tehama.
“Kupitia klabu hizi za kidijiti tunajenga jamii yenye ufahamu wa teknolojia ya kidijiti na iliyo na taarifa na fursa zake “amesema Dk.Bakari .
Aliongeza kuwa dunia ipo katika zama za taarifa zinazoenda sambamba na uchumi wa kidijiti .
Aidha amesema katika zama hizi ambazo zinajulikana kama zama za mapinduzi ya nne ya viwanda tehama ndiyo nyezo muhimu katika maendeleo ya kiuchumi na kijamii.