Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) imetoa tahadhari kuhusu uwepo wa mvua nyingi katika kipindi cha Novemba 2023 hadi Januari 2024 kwenye eneo kubwa la Tanzania. Kaimu Mkurugenzi Mkuu TMA, Dk. Ladislaus Chang’a, amesema kipindi cha nusu ya msimu (Novemba 2023 hadi Januari 2024) kinatarajiwa kuwa na mvua nyingi ikilinganishwa na nusu ya pili (Februari hadi Aprili 2024).
Amesema mvua za juu ya wastani hadi wastani zinatarajiwa katika maeneo ya kusini mwa Mkoa wa Morogoro, Mikoa ya Iringa, Lindi, Mtwara, Singida, Dodoma, kaskazini mwa Mkoa wa Katavi, Kigoma na Tabora, lakini pia mvua za wastani hadi juu ya wastani zinatarajiwa kusini mwa Mkoa wa Katavi, Mikoa ya Njombe, Rukwa, Songwe, Mbeya na Ruvuma.
Dk. Chang’a ambaye pia ni Makamu Mwenyekiti Jopo la Kimataifa la Sayansi ya Mabadiliko ya Hali ya Hewa na Tabia Nchi (IPCC), amesema uwepo wa El – Niño unatarajiwa kuwa na mchango mkubwa katika mvua za msimu.