Maelfu ya watu waliandamana kote duniani siku ya Jumamosi, kuunga mkono Wapalestina wa Ukanda wa Ghaza unaokumbwa na mashambulizi ya Israel ya kulipiza kisasi shambulio la wanamapambano wa Hamas tarehe 7 Oktoba.
Nchini Senegal, watu zaid ya 200 walikusanyika nje ya Msikiti Mkuu huko Dakar, wakiwa na bendera ya Palestina na mabango ya kulaani mauaji ya halaiki yanayofanywa na utawala ghasibu wa Israel katika Ukanda wa Ghaza.
Mmoja wa waandamanaji amesikika akisema: “Niko hapa leo, kama walivyo watu wote kute duniani, kutoa wito wa kusitishwa mauaji ya Wapalestina huko Ghaza, kuiambia Israel ikomeshe mauaji hayo, kuiambia Israel kwamba watoto wanaowaua hawakufanya kosa lolote na kuitaka iheshimu sheria za kimataifa.
Mimi siko hapa kama Mwarabu au Mwislamu, niko hapa kama mwanadamu kwa sababu ya unyama ambao unaoendelezwa huko Ghaza. Niko hapa leo kuwaunga mkono wakazi wa Ghaza na kuiambia Isreal ikomeshe ubaguzi wa rangi, mauaji ya halaiki na mauaji ya kizazi.”
Jeshi la Israel limekuwa litekeleza oparesheni za nchi kavu sambamba na mashambulizi yake ya anga, na Jumapili kwa mara nyingine tena iliwataka watu wa Ghaza kuondoka katika eneo hilo ili kuepuka kuuawa.