Watu 14 wamepoteza maisha kutokana na mafuriko yaliyosababishwa na mvua kubwa zinazoendelea kunyesha nchini Somalia.
Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Kuratibu Masuala ya Kibinadamu (OCHA) imesema hayo katika kikao na waandishi wabari mjini Mogadishu na kuongeza kuwa, marufiko hayo yameathiri watu zaidi ya laki nne.
Taasisi hiyo ya Umoja wa Mataifa imesema watu zaidi ya 47,000 wamehamishiwa katika nyanda za juu ili kuwaepusha na hatari ya mafuriko hayo. Imesema aghalabu ya walioathiriwa na mafuriko hayo ni wakazi wa majimbo ya Jubaland na Kusini Magharibi.
OCHA ilitangaza hivi karibuni habari ya watu 107,000 kuyahama makazi yao katika wilaya ya Baidoa ya kusini magharibi mwa Somalia kutokana na mafuriko.
Aidha nyumba kadhaa zimefunikwa na maji yakiwemo makazi ya muda ya yaliyokuwa yamewapa hifadhi wakimbizi zaidi ya 86,700 wa ndani huko Baidoa. Mvua hizi za msimu zilianza kunyesha mwezi uliopita wa Oktoba na zinatazamiwa kuendelea hadi Disemba.
Kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa, mvua hizo kubwa na mafuriko yamekuja kufuatia misimu mitano ya ukame ambayo imesababisha vifo vya zaidi ya Wasomali milioni 1.4 na mifugo milioni 3.8 tangu katikati ya mwaka 2021.
Umoja wa Mataifa unakadiria kuwa watu milioni 1.2 na hekta milioni 1.5 za ardhi yenye rotuba wako katika hatari kubwa kutokana na mafuriko nchini Somalia.