Shirika la Afya Duniani (WHO) limesema kuwa, Ethiopia imevunja rekodi ya idadi kubwa zaidi ya wagonjwa wa malaria katika kipindi cha miaka saba iliyopita.
Shirika hilo la Afya Duniani limetegemea ripoti ya kituo cha afya cha Ethiopia kwa kifupi (EHCB) ikisema kwamba, kumekuwa na ongezeko la asilimia 25 la kesi za ugonjwa wa malaria ndani ya muda wa mwezi mmoja ulopita katika nchi hiyo ya mashariki mwa Afrika.
Hadi tarehe 29 Oktoba, wilaya 901 kote Ethiopia ukiondoa wilaya za mkoa wa Amhara ambao ndio wa pili kwa kuwa na wakazi wengi zaidi nchini Ethiopia, zilikuwa zimeripoti angalau kesi moja ya ugonjwa wa malaria, na kufanya idadi ya kesi za ugonjwa wa malaria zilizoripotiwa nchi nzima kufikia 2,873,114 (milioni mbili na laki nane na 73,114).
Ripoti hiyo imeongeza kuwa, zaidi ya asilimia 50 ya kesi hizo zimeripotiwa katika mkoa wa Oromia ambalo ndilo eneo kubwa zaidi la Ethiopia.
Mwanzoni mwa mwezi uliopita wa Agosti, Ethiopia ilitangaza mripuko mkubwa wa ugonjwa wa malaria katika jimbo la Oromia, huku maafisa wa afya wakiripoti kesi nyingine nyingi za ugonjwa huo katika wilaya za Begi na Kondala za eneo hilo lenye migogoro ya kivita la Wollega Magharibi.
Jawar Qasim, mkuu wa Idara ya Afya ya Oromia alisema wakati huo kwamba ugonjwa huo umeathiri vibaya watu katika kanda 16 za Oromia, na kuna ongezeko la asilimia 168 mwaka huu ikilinganishwa na mwaka uliopita.