Zaidi ya watu 300,000 jimboni Kivu Kaskazini mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC wamefurushwa makwao mwezi Oktoba pekee kutokana na mapigano yanayozidi kushadidi kwenye eneo hilo.
Msemaji wa Umoja wa Mataifa Stephane Dujarric amewaambia waandishi wa habari jijini New York kwamba idadi hii inafanya idadi ya watu waliofurushwa makwao eneo la Mashariki mwa nchi hiyo kufikia milioni 6.
Mapigano yanaenda sambamba na milipuko ya mara kwa mara ya ugonjwa wa kipindupindu na surua.
Licha ya hali kuwa tete mashariki mwa DRC, Dujarric amesema Umoja wa Mataifa pamoja na wadau wake wamefikisha misaada kwa watu wapatao milioni 3, ambapo miongoni mwake ni misaada ya chakula kwa watu milioni 1.9 kwenye eneo hilo.
Hata hivyo, “kama tulivyosema mara kadhaa, suala la kufikia wahitaji linasalia kuwa changamoto kubwa kutokana na ghasia zinazoendelea kwenye mji wa Beni,” amesema msemaji huyo wa Umoja wa Mataifa.
Ghasia hizo zimesababisha watoa misaada kusitisha kwa muda shughuli zao na hivyo kuacha watu 140,000 bila uwezo wa kupata misaada ya kiutu.
Ombi la mwaka huu la kusaidia DRC la dola bilioni 2.3 limefadhiliwa kwa asilimia 36 pekee, na hivyo fedha zaidi zinahitajika.