Rais wa Kenya William Ruto, Naibu wake Rigathi Gachagua na Waziri wa Ulinzi wa nchi hiyo, Aden Duale, wametangaza vita kali dhidi ya kundi la Al-Shabaab, ambalo limekuwa likifanya mashambulio katika Kaunti za kaskazini mwa Kenya, ikiwemo kaunti ya Lamu.
Akizungumza katika kisiwa cha Kizingitini huko Lamu Mashariki wakati wa ziara ya kuzindua miradi ya maendeleo, Rais Ruto alisisitiza kuwa, utawala wake hautaruhusu magaidi kuendelea kufanya mashambulio nchini humo, na kuongeza kuwa tayari amezungumza na mawaziri, hasa wanaohusika na usalama wa ndani na ulinzi wa nchi, kuhakikisha kuwa vita dhidi ya Al-Shabaab inaongezewa nguvu.
Naibu wa Rais Rigathi Gachagua naye aliwasihi wananchi wa Lamu na viongozi kuepuka kugawanywa na magaidi na badala yake waungane kukabiliana na magaidi hao.
Kwa upande wake, Waziri wa Ulinzi, Aden Duale alisema serikali iko makini katika kupambana na wapiganaji wa kundi la Al-Shabaab ndani ya Somalia na pia kwenye mpaka kati ya Somalia na Kenya.