Luis Diaz alirejea katika timu ya Liverpool na kufunga bao la kusawazisha dakika za lala salama katika mechi yake ya Ligi ya Premia dhidi ya Luton Jumapili, huku baba yake akiwa bado hayupo baada ya kutekwa nyara na kundi la wapiganaji nchini Colombia.
Diaz alikuwa amekosa mechi mbili za mwisho za Liverpool lakini alifanya mazoezi tangu Alhamisi na alichaguliwa kwenye benchi kwa mechi hiyo iliyofanyika Kenilworth Road. Aliingia kwenye mchezo dakika ya 83 na kufunga bao katika dakika ya tano ya dakika za lala salama na kuihakikishia timu yake sare ya 1-1.
Alifunua fulana yenye maneno “Libertad Para Papa” (“Uhuru kwa baba”) baada ya bao hilo.
Diaz alifuata hilo na chapisho kwenye Instagram baadaye Jumapili.
Ilisomeka, “Leo mwanasoka haongei na wewe. Leo Lucho Diaz, mwana wa Luis Manuel Diaz, anazungumza nawe. baba yangu, ni mfanyakazi asiyechoka, nguzo katika familia na ametekwa nyara. Ninaomba ELN kuachiliwa mara moja kwa baba yangu, na ninaomba mashirika ya kimataifa kufanya kazi pamoja kwa ajili ya uhuru wake.
“Kila sekunde, kila dakika, uchungu wetu unakua. Mama yangu, kaka zangu na mimi tumekata tamaa, tumefadhaika na hatuna maneno ya kuelezea kile tunachohisi. Mateso haya yataisha tu tutakapokuwa naye nyumbani. Ninakuomba umuachilie mara moja, kwa kuheshimu uadilifu wake na kumaliza kungoja huku kwa maumivu haraka iwezekanavyo.”
Wazazi wote wawili wa Diaz walitekwa nyara katika mji mdogo wa Colombia wa Barrancas wikendi iliyopita, ingawa mama yake aliokolewa saa chache na polisi.
Serikali ya Colombia ilisema Alhamisi kwamba kikundi cha waasi cha National Liberation Army, kinachojulikana kama ELN, kilihusika na utekaji nyara huo.
“Kwenye uwanja wa mazoezi alikuwa sawa, uwanjani alikuwa sawa, kwa hiyo ndiyo sababu yuko hapa,” meneja wa Liverpool Jurgen Klopp alikuwa amesema kuhusu mchezaji wake kabla ya mchezo huo.
“Dalili zote anazopata, kwa kadri ninavyoelewa, ni nzuri sana,” Klopp alisema kuhusu hali ya baba ya Diaz. “Mazungumzo yanaendelea lakini bado mazuri na ndiyo maana (Diaz) alitaka kuwa sehemu ya timu.”