Waasi wanaotaka kujitenga waliwauwa karibu watu 20, wakiwemo wanawake na watoto, katika shambulio dhidi ya kijiji kimoja katika maeneo yenye machafuko ya Anglophone nchini Cameroon, serikali ilisema Jumatatu (Nov. 06).
“Kulikuwa na wanaume, wanawake na watoto, zaidi ya 20 waliuawa,” waziri katika ofisi ya rais Mengot Victor Arrey-Nkongho aliambia redio ya umma. “Haivumiliki.”
Shambulio hilo la usiku lilitokea katika kijiji cha Egbekaw magharibi mwa Cameroon – eneo la mapigano makali kati ya waasi na vikosi vya serikali kwa miaka saba.
Hakuna kundi lililodai kuhusika na shambulio hilo.
Kulingana na shirika la utangazaji la CRTV Mkuu wa mkoa wa Manyu, Viang Mekala, alitangaza kuwa uchunguzi umeanzishwa ili kubaini wahalifu hao. Watu 7 walijeruhiwa.
Mikoa ya Cameroon inayozungumza Kiingereza hasa kaskazini-magharibi na kusini-magharibi imekumbwa na mzozo tangu watu wanaotaka kujitenga walipotangaza uhuru wake mwaka 2017.