Wizara ya Maliasili na Utalii, kupitia Bodi ya Utalii Tanzania (TTB) katika kuhakikisha kuwa inatimiza malengo iliyojiwekea kama nchi ya kupata watalii milioni tano na kuliingizia taifa zaidi ya dola za kimarekani bilioni sita kwa mwaka, hivi sasa inashiriki maonesho makubwa ya utalii duniani ya World Travel Market (WTM) yanayoendelea nchini Uingereza ili kutangaza urithi na hazina kubwa ya vivutio vya utalii ambavyo vinapatikana Tanzania.
Akizungumza leo Novemba 7, 2023 jijini London kuhusu mafanikio ya ushiriki wa Tanzania katika maonesho ya WTM ya mwaka huu, kiongozi anayeongoza ujumbe wa TTB katika maonesho hayo bw.Damasi Mfugale ambaye ndiye Mtendaji Mkuu wa TTB amesema tayari wameshafanya majadiliano na kushawishi makampuni kadhaa makubwa duniani kuwaleta watalii nchini mapema hapo mwakani.
“Kama unavyofahamu China ni miongoni mwa soko letu la kimkakati, tayari katika maonesho haya tumekutana nao kupitia kwa mdau kubwa anayejulikana kama Marcus Lee tumekubaliana mambo kadhaa na tayari maandalizi ya kuwaleta watalii China ikiwepo mafunzo yajulikakanayo kama China ready program , programu inayotegemea kuanza mwezi Februari mwakani 2024”. Amefafanua Mfugale
Aidha, amesema mpango uliopo ni kukamilisha kufanya ushawishi na majadiliano na makampuni yote makubwa ya wapeleka watalii au ya usafirishaji watalii kutoka kwenye vitovu vya masoko ya utalii duniani kwenye mabara yote yanayoshiriki maonesho haya.
Ameyataja baadhi ya makampuni makubwa ya kimkakati wanayoendelea kufanya nao majadiliano kuwa ni pamoja na KUONI, TUI, Expedia, China Truly Travel Hey & Jervis (UK) Africa Explorers (Italy) na Thomson (UK).
WTM ni miongoni mwa maonesho makubwa ya utalii duniani ambayo yametimiza miaka 43 toka kuanzishwa kwake, kwa sasa huwakutanisha zaidi ya wadau 700 kutoka sehemu mbalimbali duniani kwa maana ya wauzaji, wanunuzi na waandishi na wanahabari.