Ripoti ya ugonjwa wa Kifua Kikuu (TB) ya mwaka 2023 iliyotolewa jana na Shirika la Afya Duniani WHO inaonesha kuwa, mwaka 2022 watu milioni 1.3 walifariki kwa magonjwa yanayohusiana na Kifua Kikuu.
Ripoti imesema jumuiya ya kimataifa bado inatakiwa kuongeza juhudi katika kukinga na kutibu ugonjwa huo.
Kwa mujibu wa ripoti hiyo, tangu mwaka 2000, juhudi za kupambana na Kifua Kikuu duniani zimeokoa maisha ya watu zaidi ya milioni 75.
Mwaka 2022 jumla ya watu milioni 7.5 walithibitishwa kuambukizwa ugonjwa huo, idadi ambayo ni kubwa zaidi kwa mwaka tangu WHO ianze usimamizi wa Kifua Kikuu mwaka 1995.
Ripoti hiyo inasema, maendeleo kadhaa yamepatikana kwenye tiba, dawa na chanjo ya Kifua Kikuu, lakini kiwango cha uwekezaji kwenye sekta hiyo kimezuia maendeleo zaidi.