Urusi ilisema siku ya Jumatano kuwa imeweka katika orodha yake inayotafutwa jaji mwingine wa mahakama ya kimataifa ya uhalifu, inayotaka kukamatwa kwa Rais Vladimir Putin kutokana na mzozo wa Ukraine.
“Inatafutwa katika mfumo wa uchunguzi wa jinai,” ilisema notisi katika hifadhidata ya wizara ya mambo ya ndani, ikirejelea Sergio Gerarde Ugaldo Godinez, jaji wa Costa Rica katika ICC yenye makao yake The Hague.
Notisi hiyo haikutoa maelezo ya kina kuhusu tuhuma dhidi ya Godinez.
Mwezi Machi, ICC ilitangaza hati ya kukamatwa kwa Putin kwa tuhuma za uhalifu wa kivita za kuwafukuza watoto wa Ukraine kinyume cha sheria.
ICC pia ilitoa waranti dhidi ya Maria Lvova-Belova, kamishna wa rais wa Urusi wa haki za watoto, kwa mashtaka sawa.
Urusi, ambayo si mwanachama wa ICC, inasisitiza kuwa waranti dhidi ya Putin ni “batili”, AFP inaripoti.