Takribani watu Laki Mbili nchini wana ugonjwa wa Selimundu (Sickle Cell) huku watoto Elfu Kumi na Moja (11,000) huzaliwa wakiwa na ugonjwa wa Selimundu unaohusisha kurithi vinasaba toka kwa wazazi ndani ya mwaka mmoja.
Hayo yamebainishwa leo Bungeni Jijini Dodoma na Naibu Waziri wa Afya, Dkt. Godwin Mollel wakati akijibu swali Namba 124 kwa niaba ya Waziri wa Afya Mhe. Ummy Mwalimu kutoka kwa Mbunge wa Viti Malum Mhe. Fatma Hassan Toufiq aliyeuliza ni Watanzania wangapi wenye tatizo la Sickle cell na ni Mikoa mingapi imeathiriwa sana na ugonjwa huu.
Dkt.Mollel amesema kuwa Mikoa iliyoathiriwa zaidi na ugonjwa wa Selimundu ni Mwanza, Tabora, Kigoma, Mara, Dar es Salaam pamoja na Pwani.
“Tafiti zinaonesha sehemu zenye maambukizi ya ugonjwa wa malaria kwa wingi ndizo ambazo pia zina wagonjwa wengi wa Selimundu”. Ameeleza Dkt. Mollel
Amesema, Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania chini ya kiongozi makini Rais Samia Suluhu Hassan hivi karibuni iliamua kuwekeza shilingi bilioni 2.7 ili kuanzisha huduma ya upandikizaji uloto na kupunguza gharama za matibabu ya Selimundu kwa wananchi.
“Kuimarika kwa huduma za kibingwa na bobezi nchini kumepunguza gharama kubwa iliyokuwa inatumiwa na Serikali ili kuwezesha Watanzania wenye uhitaji kupata huduma hizo nje ya nchi, huduma hii ya upandikizaji uloto ikitolewa katika hospitali zetu hapa nchini, itagharimu shilingi milioni 50 hadi 55 kwa mgonjwa mmoja”. Amesema Dkt. Mollel.
Aidha, kwa mujibu wa takwimu za Mfumo wa Taarifa za Uendeshaji wa Huduma za Afya (MTUHA) zinaonesha kuwa jumla ya wagonjwa Elfu 86,990 wa Sickle Cell walihudumiwa kwa mwaka 2022.