Waziri wa Ujenzi, Innocent Bashungwa, amekutana na kufanya mazungumzo na Uongozi wa kampuni ya Beijing Construction Engineering Group Ltd (BCEG), inayojenga mradi wa Kiwanja cha ndege cha Kimataifa cha Msalato jijini Dodoma kujadili masuala mbalimbali kuhusu mradi huo.
Mazungumzo hayo yamefanyika leo tarehe 07 Novemba, 2023 jijini Dodoma ambapo pamoja na mambo mengine Waziri Bashungwa pamoja na uongozi huo walijadili kwa undani kuhusu changamoto za mradi huo na namna ya kufanya maboresho ili kuhakikisha mradi huo unakamilika kwa wakati ifikapo Desemba, 2023.
Kikao hicho kimeshirikisha Viongozi na wataalam kutoka Wizara ya Ujenzi, Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) na Viongozi kutoka Kampuni ya Kikandarasi a BCEG kutoka China.